< Yoshua 8 >
1 Yahweh akamwambia Yoshua, “Usiogope; usivunjike moyo. Chukua pamoja nawe watu wa vita. Pandeni kwenda Ai. Tazama nimemtia mkononi mwako mfalme wa Ai, watu wake, mji wake na nchi yake.
Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake.
2 Mtafanya hivyo pia huko Ai na mfalme wake kama mlivyofanya kwa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mtachukua nyara na mifugo kwa ajili yenu. Pangeni mashambulizi ya uviziaji nyuma ya mji.”
Utafanya Ai na mfalme wake kama ulivyofanya kwa mji wa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kuchukua mateka wake na mifugo wake, kwa ajili yenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”
3 Basi Yoshua aliinuka na akawachukua kwenda Ai watu wote wa vita. Kisha Yoshua akachagua watu elfu thelathini - wenye nguvu na ujasiri - na aliwatuma waende wakati wa usiku.
Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua watu mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku
4 Aliwaamuru, “Tazama, mtalala katika hali ya mashambulizi ya uviziaji dhidi ya mji, kwa nyuma yake. Usiende mbali sana na mji, lakini ninyi nyote muwe tayari.
akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho.
5 Mimi pamoja na watu wote walio pamoja nami tutaukaribia mji. Na wakati watakapokuja kutushambulia sisi, tutawakimbia kama tulivyofanya hapo mwanzo.
Mimi na watu walio pamoja nami, tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutawakimbia.
6 Watatoka nje watukimbize mpaka hapo tutakapokuwa tumewavuta mbali sana na mji, watasema, “Wanatukimbia kama walivyofanya mara ya mwisho.' Hivyo tutawakimbia na kwenda mbali.
Watatufuatilia mpaka tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia,
7 Kisha mtapanda kutoka sehemu mliyojificha, na mtauteka mji. Yahweh Mungu wenu atawapa mkononi mwenu.
ninyi inawapasa mwinuke mtoke huko mafichoni na kuuteka mji. Bwana Mungu wenu atautia mkononi mwenu.
8 Tazama nimewaamuru, mtakapouteka mji, mtauchoma moto. Mtayafanya haya wakati mtakapotii agizo lililotolewa katika neno la Yahweh.”
Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Bwana alivyoamuru. Angalieni, nimewaagiza.”
9 Yoshua akawatuma, na wakaenda sehemu ya uviziajia, na wakajificha kati ya Betheli na Ai sehemu ya magharibi ya Ai. Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku ule.
Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.
10 Yoshua aliamka asubuhi na mapema na akawaandaa tayari wanajeshi wake, Yoshua na wazee wa Israeli walishambuliwa watu wa Ai.
Asubuhi na mapema siku iliyofuatia, Yoshua akawakutanisha watu wake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawa mbele ya watu kwenda Ai.
11 Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda na kuukaribia mji. Walisogea karibu na mji na wakapiga kambi sehemu ya kasikazini mwa Ai. Kulikuwa na bonde kati yao na Ai.
Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji.
12 Alichukua watu wapatao elfu tano hivi na akawaweka katika hali ya kuvizia katika upande wa magharibi mwa mji kati ya Betheli na Ai.
Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka katika uavizi kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji.
13 Waliwapanga wanajeshi wote, jeshi kuu katika upande wa kasikazini mwa mji, na walinzi wa nyuma upande wa magharibi mwa mji. Yoshua alilala bondeni usiku ule.
Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.
14 Na ilikuwa alipoona hilo mfalme wa Ai, yeye pamoja na jeshi lake, waliamka asubuhi na mapema na walitoka kwa haraka kwenda kuwashambulia Israeli katika eneo linalokabili bonde la Mto Yordani. Hakujua kuwa kulikuwa na shambulizi la kuvizia lilikuwa linasubiria kushambulia kutokea kwa nyuma ya mji.
Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na watu wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema, ili kukutana na Israeli katika vita mahali fulani panapotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji.
15 Yoshua na Waisraeli wote walikubali wenyewe kushindwa mbele yenu, na wakakimbia kuelekea nyikani.
Yoshua na Israeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani.
16 Watu wote waliokuwa kwenye mji waliitwa kwa pamoja waende mbele yao, na walienda mbele ya Yoshua na kwa jinsi hiyo walivutwa mbali na mji.
Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji.
17 Hapakuwa na mtu mme aliyesalia Ai na Betheli ambaye alikuwa hajaenda nje kuwafuatilia waisraeli. Na walipokuwa wanawafuatilia Waisraeli, Wakatoka na waliuacha mji wazi.
Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.
18 Yahweh akamwambia Yoshua, “Nyosha mkuki huo ulio mkononi mwako kuelekea Ai, kwa kuwa nitaitia Ai mikononi mwako.” Yoshua akaunyosha mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea mji.
Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai.
19 Wanajeshi waliojificha katika hali ya kuvizia walitoka upesi katika eneo lao mara tu alipounyosha mkono wake. Walikimbia mbio na kuuingia mji na kuuteka. Na kwa haraka wakauchoma moto mji.
Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mavizioni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbilia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.
20 Watu wa Ai waligeuka na kuangalia nyuma. Waliona moshi kutoka katika mji ukipanda kwenda angani, na hawakuweza kutoroka kwa njia hii au ile. Kwa kuwa wanajeshi wa Israelei waliokuwa wamekimbia katika nyika, sasa walirudi kuwakabili wale waliokuwa wanawafuatilia.
Watu wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wanawakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao.
21 Na wakati Yoshua na Israeli wote walipoona kuwa wale watu wa kuvizia wameuteka mji kwa ule moshi uliokuwa ukipanda, waligeuka nyuma na kuwaua watu wa Ai.
Basi Yoshua na Israeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kutoka kwenye mji, wakawageukia watu wa Ai na kuwashambulia.
22 Na wanajeshi wengine wa Israeli, wale waliokuwa wameingia ndani ya mji, walitoka nje ili kuwashambulia. Hivyo, watu wa Ai walikamatwa katikati ya majeshi ya Israeli, baadhi katika upande huu na wengine katika upande ule.
Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka.
23 Lakini walimhifadhi mfalme wa Ai, ambaye walimteka akiwa hai, na kisha wakamleta kwa Yoshua.
Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.
24 Ilikuwa baada ya Israeli walipokuwa wamemaliza kuuwaua wenyeji wote wa Ai katika uwanda kariibu na nyika mahali walipowafuata, na baada ya wao wote, hata yule wa mwisho, walipokuwa wamekwisha kulala kwa ncha ya upanga, Waisraeli wote walirudi Ai. Waliuteka mji kwa ncha ya upanga.
Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini.
25 Wale wote walikufa siku hiyo walikuwa watu elfu kumi na mbili elfu, wanaume na wanawake, wote ni watu wa Ai.
Watu kumi na mbili elfu, waume kwa wake, waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai.
26 Yoshua hakuukunja mkono wake ambao alikuwa ameunyosha huku akishikilia mkuki wake, mpaka pale alipowateketeza kabisa watu wote wa Ai.
Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai.
27 Waisraeli walichukua tu wanyama na nyara kutoka katika mji kwa ajili yao wenyewe, kama Yahweh alivyokuwa amemwagiza Yoshua.
Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Yoshua.
28 Yoshua aliichoma Ai na kuigeuza kuwa kichuguu cha mapango. Ni mahali palipoachwa ukiwa hata leo.
Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo.
29 Alimtundika mfalme wa Ai juu ya mti mpaka jioni. Na jua lilipokuwa linaenda kuzama, Yoshua aliwaagiza na wakautoa mwili wa mfalme wakaushusha chini ya mti na kuutupa mbele ya malango ya mji. Huko wakaweka kichuguu kikubwa cha mawe juu yake. Kichuguu hicho kimebaki huko hata leo.
Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo mpaka jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe makubwa mengi juu yake, ambayo yamesalia mpaka leo.
30 Kisha Yoshua akajenga madhabahu kwa Yahweh, Mungu wa Israeli katika Mlima wa Ebali,
Kisha Yoshua akajenga madhabahu ya Bwana, Mungu wa Israeli, katika Mlima wa Ebali,
31 kama vile Musa mtumishi wa Yahweh alivyowaagiza watu wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Musa: “Madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna mtu yeyote aliyetumia zana ya chuma.” Na allimtolea Yahweh sadaka ya kuteketezwa juu yake na wakatoa sadaka ya amani.
kama Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani.
32 Na huko aliandika juu ya mawe nakala ya sheria za Musa mbele ya watu wa Israeli.
Pale, mbele ya Waisraeli Yoshua akanakili juu ya hayo mawe sheria ya Mose, aliyokuwa ameiandika.
33 Waisraeli wote, wazee wao, maafisa, na waamuzi wao walisimama katika sehemu mbili za sanduku mbele ya makuhani na Walawi ambao hulibeba sanduku la Agano la Yahweh - wageni pamoja na wazalia, nusu yao walisimama mbele ya Mlima Gerizimu na nusu walisimama mbele ya Mlima Ebali. Waliwabariki watu wa Israeli kama Musa mtumishi wa Yahweh alivyowaagiza hapo mwanzo.
Israeli yote, wageni na wazawa sawasawa, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Bwana, wakiwaelekea wale waliokuwa wamelichukua, yaani makuhani, ambao ni Walawi. Nusu ya watu ilisimama mbele ya Mlima Gerizimu na nusu hiyo ingine ikasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.
34 Baada ya hayo, Yoshua alisoma maneno yote ya sheria, baraka na laana, kama zilivyoandikwa katika kitabu cha sheria.
Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.
35 Halikusalia hata neno moja katika yote ambayo Musa alimwagiza Yoshua ambalo halikusomwa mbele ya kusanyiko la Waisraeli lilojumuisha wanawake, watoto wadogo na wageni walioishi miongoni mwao.
Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Mose alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakulisomea kusanyiko lote la Israeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.