< Yoshua 6 >
1 Basi, milango yote ya Yeriko ilikuwa imefungwa kwasababu ya jeshi la Israeli. Hapakuwa na mtu wa kutoka nje au kuingia ndani.
Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa ajili ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
2 Yahweh akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeweka Yeriko katika mkono wako, mfalme wake pamoja na wanajeshi wake waliofunzwa.
Kisha Bwana akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita.
3 Ni lazima kutembea kwa kuuzunguka mji, wanaume wote wa vita wauzunguke mji mara moja. Ni lazima mfanye hivi kwa siku sita.
Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita.
4 Makuhani saba lazima wabebe tarumbeta za pembe za kondoo waume mbele za sanduku. Na katika siku ya saba, ni lazima mtembee kwa kuuzunguka mji mara saba, na makuhani lazima wapulize tarumbeta.
Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo.
5 Kisha watapuliza pembe za kondoo waume kwa nguvu kuu, na mtakaposikia sauti za tarumbeta watu wote na wapige kelele kwa mshindo mkuu, na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale. Wanajeshi ni lazime washambulie, kila mmoja eende mbele moja kwa moja.
Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele.”
6 Ndipo Yoshua mwana wa Nuni, aliwaita makuhani na kuwaambia, “Lichukueni sanduku la agano, na waacheni makuhani saba wabebe tarumbeta za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Yahweh.”
Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la Bwana na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.”
7 Yoshua aliwaambia watu, “Nendeni na mkatembee kuuzunguka mji, na watu wa vita wataenda mbele ya sanduku la Yahweh.”
Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Bwana.”
8 Makuhani saba walibeba tarumbeta saba za pembe za kondoo mbele ya Yahweh kama Yoshua alivyowaambia watu. Na walivyokuwa akiendelea mbele, walipuliza tarumbeta.
Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba wenye kuzibeba zile baragumu saba mbele za Bwana, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la Bwana likawafuata.
9 Sanduku la Yahweh liliwafuata kwa nyuma yao. Watu wa vita walitembea mbele ya makuhani, na walipuliza tarumbeta zao, lakini walinzi wa nyuma walilifuata sanduku kwa nyuma, na makuhani waliendelea kupuliza tarumbeta zao.
Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa.
10 Lakini Yoshua aliwaagiza watu, akisema, “Msipige kelele. Sauti yoyote isitoke vinywani mwenu mpaka siku nitakayowaambia kupiga kelele. Ndipo hapo mtakapopiga kelele.”
Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige kelele ya vita, msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote mpaka siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!”
11 Hivyo, alisababisha sanduku la Yahweh kuuzunguka mji mara moja kwa siku hiyo. Kisha wakaingia katika kambi yao, wakakaa usiku ule katika kambi.
Basi akalipeleka Sanduku la Bwana kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.
12 Basi Yoshua aliamka asubuhi na mapema, na makuhani wakalichukua sanduku la Yahweh.
Yoshua akaamka mapema asubuhi iliyofuata nao makuhani wakalichukua Sanduku la Bwana.
13 Makuhani saba waliobeba tarumbeta saba za pembe za kondoo waume walikuwa mbele ya sanduku la Yahweh, wakitembea kwa ushupavu, huku wakipuliza tarumbeta. Wanajeshi wenye silaha walikuwa wakitembea mbele yao, lakini walinzi wa nyuma walitembea nyuma ya sanduku la Yahweh, huku tarumbeta ziliendelea kupigwa.
Wale Makuhani saba wakizibeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la Bwana wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la Bwana, huku baragumu hizo zikiendelea kulia.
14 Walitembea kuuzunguka mji mara moja katika siku ya pili na kisha wakarudi kambini. Walifanya hivi kwa siku sita.
Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.
15 Ilikuwa ni katika siku ya saba ambayo waliamka mapema katika mapambazuko, na walitembea kuuzunguka mji kwa namna ile kama ilivyokuwa kawaida yao, katika siku hii walifanya mara saba.
Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba.
16 Ilikuwa ni katika siku ya saba ambapo makuhani walipiga tarumbeta, na ya kwamba Yoshua aliwaagiza watu, “Pigeni kelele! Kwa kuwa Yahweh amewapa ninyi mji.
Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipopiga baragumu kwa sauti kubwa, Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana Bwana amewapa mji huu!
17 Mji pamoja na vitu vyote ndani yake vitatengwa kwa Yahweh kwa ajili ya uharibifu. Ni Rahabu yule kahaba pekee ataishi - yeye pamoja wote waliokuwa pamoja naye katika nyumba - kwasababu aliwaficha watu tuliowatuma.
Mji huu pamoja na vyote vilivyomo ndani yake utawekwa wakfu kwa Bwana. Ila Rahabu tu, yule kahaba na wote ambao wako pamoja naye nyumbani mwake ndio watakaosalimishwa, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma.
18 Lakini kwenu, iweni waangalifu juu ya kuchukua vitu vilivyotengwa kwa ajili ya uharibifu, ili baada ya kuvitia alama kwa ajili ya kuharibiwa, msichukue hata kimoja wapo. Na kama mtafanya hivi, mtaifanya kambi ya Waisraeli iharibiwe na mtaleta matatizo katika kambi.
Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua chochote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu.
19 Fedha zote, dhahabu na vitu vilivyotengenezwa kwa shaba na chuma vilitengwa kwa ajli ya Yahweh.”
Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Bwana, lazima viletwe katika hazina yake.”
20 Hivyo, watu wakapiga kelele, na wakatoa sauti kwa kupuliza tarumbeta. Ilikuwa watu waliposikia sauti za tarumbeta, walipiga kelele kwa sauti kuu, na ukuta ulianguka chini kabisa na kwamba watu waliungia mji, kila mmoja alisonga mbele moja kwa moja. Na waliuteka mji.
Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, na katika sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.
21 Waliteketeza kabisa kila kitu kilichokuwa katika mji kwa makali ya upanga - wanaume kwa wanawake, wadogo kwa wakubwa, ng'ombe, kondoo na punda.
Wakauweka mji wakfu kwa Bwana, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, ngʼombe, kondoo na punda.
22 Kisha Yoshua akawaambia wale watu wawili walioipeleleza nchi, “Nendeni katika nyumba ya kahaba, mtoeni mwanamke na wote walio pamoja naye, kama mlivyomwapia.”
Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani kwa yule kahaba, mleteni pamoja na wote waliomo nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.”
23 Basi, vijana wale walioipeleleza nchi waliingia ndani na kumtoa Rahabu nje. Walimtoa nje baba yake, mama, kaka, na ndugu wote waliokuwa pamoja naye. waliwaleta katika sehemu ya nje ya kambi ya Waisraeli.
Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli.
24 Na ndipo waliuteketeza mji na kila kitu ndani yake. Isipokuwa fedha, dhahabu na vyombo vya fedha na chuma viliwekwa kwa hazina ya nyumba ya Yahweh.
Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwamo ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya Bwana.
25 Bali Yoshua alimruhusu Rahabu kahaba, nyumba ya baba yake, na wote waliokuwa pamoja naye waishi. Mpaka leo hivi anaishi Israeli kwasababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko.
Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na wote waliokuwa wa kwake, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.
26 Kisha katika kipindi hicho, Yoshua aliwaamuru kwa kiapo na kusema, “Alaaniwe machoni pa Yahweh mtu yule anayeujenga mji huu, Yeriko. Ataujenga msingi kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza, na kwa gharama ya mzaliwa wake wa pili atapachika milango yake.”
Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Aliyelaaniwa mbele za Bwana ni mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko: “Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume ataiweka misingi yake; kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho atayaweka malango yake.”
27 Basi Yahweh alikuwa pamoja na Yoshua, na umaarufu wake ulienea katika nchi yote.
Hivyo Bwana alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi yote.