< Yoshua 2 >

1 Kisha Yoshua mwana wa Nuni aliwatuma watu wawili kwa siri kama wapelelezi kutoka Shitimu. Akisema, “Nendeni mkaiangalie nchi, hasa Yeriko.” Walienda na wakafika katika nyumba ya kahaba ambaye jina lake ni Rahabu, na wakalala hapo.
Kisha Yoshua mwana wa Nuni kwa siri akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Kwa hiyo wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja jina lake Rahabu na kukaa humo.
2 Mfalme wa Yeriko aliambiwa, “Tazama watu wa Israeli wamekuja kuipeleleza nchi.”
Mfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.”
3 Mfalme akatuma neno kwa Rahabu kusema, “Watoe watu waliokuja kwako ambao wameingia nyumbani mwako, kwa kuwa wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
Hivyo mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
4 Lakini mwanamke alikuwa amekwisha kuwachukua wale watu wawili na kuwaficha. Na akasema, “Ndiyo, watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka.
Lakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka.
5 Ilipokuwa jioni wakati wa kufungwa kwa lango la mji, waliondoka. Sijui mahali walikoelekea. Mnaweza kuwakamata kama mtawafuata upesi.
Kulipoingia giza, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui njia waliyoiendea. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.”
6 Lakini yeye aliwapandisha juu darini na kuwaficha kwa mabua ya kitani ambayo alikuwa ameyalaza darini.
(Lakini alikuwa amewapandisha darini akawafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.)
7 Hivyo, watu waliwafuatilia njiani iliyoeleka katika vivuko vya Yordani. Na milango ilifungwa mara tu baada ya wale watu waliofuata kutoka nje.
Basi hao watu wakaondoka kuwafuatilia hao wapelelezi katika njia ile inayoelekea vivuko vya Yordani, mara tu wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.
8 Wale wanaume walikuwa hajalala usiku, wakati alipowaendea kule darini.
Kabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini,
9 Akawaambia, “Ninajua kwamba Yahweh amewapa ninyi nchi na kwamba hofu juu yenu imetuingia. Watu wote wanaoishi katika nchi watayeyuka mbele yenu.
akawaambia, “Ninajua kuwa Bwana amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote waishio katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu.
10 Tumesikia jinsi ambavyo Yahweh alivyokausha maji ya Bahari ya Mianzi kwa ajili yenu wakati mkitoka Misri. Na tumesikia mlichokifanya kwa wafalme wawili wa Waamori walioko upande mwingine wa Yordani - Sihoni na Ogu - ambao mmewaangamiza kabisa.
Tumesikia jinsi Bwana alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa.
11 Mara tu tuliposikia, mioyo yetu iliyeyuka na hapakuwa na ujasiri wowote uliosalia kwa mtu yeyote - kwa kuwa Yahweh Mungu wenu, ni Mungu aliye juu mbinguni na chini duniani.
Tuliposikia juu ya hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na duniani chini.
12 Sasa basi, tafadhali mniapie kwa Yahweh kwamba kama nilivyokuwa mwema kweu, nanyi pia mtaitendea mema nyumba ya baba yangu. Nipeni ishara ya uhakika
Sasa basi, tafadhali niapieni kwa Bwana, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu
13 kwamba mtanihifadhi maisha ya baba, mama, kaka, dada zangu na famiie zao, na kwamba mtatuokoa kutoka katika kifo.
kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”
14 Wanaume wakamjibu, “maisha yetu kwa ajili ya yenu, hata kifo! Kama hamtasema habari zetu, na Yahweh akisha kutupa nchi hii, tutakuwa wenye huruma na waaminifu kwenu.”
Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”
15 hivyo aliwashusha chini kwa kupitia dirishani kwa kutumia kamba. Nyumba ambayo alikuwa anaishi ilijengwa katika ukuta wa mji.
Kisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji.
16 Akawaambia, “Nendeni milimani la sivyo watu waliowafuata watawaona. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watu waliowafuata watakaporudi. Kisha nendeni zenu.”
Alikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”
17 Wanaume wakamwambia, “Hatutakuwa tumefungwa na ahadi ulizotufanya tuape mbele zako, kama hautalifanya hili.
Wale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga,
18 Tutakapokuja katika nchi, ni lazima uifunge kamba hii nyekundu katika dirisha ulilotushushia chini, na utawakusanya katika nyumba baba yako, mama yako, kaka zako na wote wa nyumba ya baba yako.
isipokuwa, hapo tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako.
19 Na yeyote aendaye mtaani nje ya milango ya nyumba yako, damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao na hatutakuwa na hatia yoyote. Lakini kama mkono utanyoshwa juu ya mtu yeyote aliye pamoja nawe katika nyumba, damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu.
Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, kama mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu.
20 Na ikiwa utaongea juu ya suala letu, tutakuwa huru dhidi ya kiapo ulichotuapisha.
Lakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kwenye kiapo hiki ulichotufanya tuape.”
21 Rahabu akawajibu, “Yote mliyosema nayatimie.” Akawatoa mbali na wakaondoka. Kisha akaifunga kamba nyekundu katika dirisha.
Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
22 Wakaondoka na kwenda juu milimani na walikaa huko kwa siku tatu hadi pale wale waliowafuatilia waliporudi. Wale waliowafuata walitafuta njiani pote bila kuwaona.
Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata.
23 Wale watu wawili walirudi na kuvuka mto na wakafika kwa Yoshua mwana wa Nuni, na walimwambia kila kitu kilichotokea kwao.
Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata.
24 Nao wakasema kwa Joshua, “kwa kweli Yahweh ametupa nchi hii. Wenyeji wote wa nchi wanayeyuka kwasababu yetu.
Wakamwambia Yoshua, “Hakika Bwana ametupa nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”

< Yoshua 2 >