< Ayubu 39 >
1 Je unajua ni wakati gani mbuzi mwitu huzaa watoto wao katika miamba? Je waweza kuwangalia paa wakati wanapozaa watoto wao?
“Je, wajua ni wakati gani mbuzi wa mlimani wanapozaa? Je, watambua ni wakati gani kulungu jike azaapo mtoto wake?
2 Waweza kuhesabu miezi ya kuchukua mimba? Je unaujua muda ambao huzaa watoto wao?
Je, waweza kuhesabu miezi hadi wazaapo? Je, unajua majira yao ya kuzaa?
3 Wanainama chini na kuzaa watoto wao, na kisha maumivu yao ya uzazi yanaishi.
Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao; utungu wa kuzaa unakoma.
4 Watoto wao huwa na nguvu na kukua katika uwanda wa wazi; hutoka nje na hawarudi tena.
Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani; huenda zao wala hawarudi tena.
5 Ni nani huwaacha punda mwitu waende huru? Je nani amevilegeza vifungo vya punda wepesi,
“Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru? Ni nani aliyezifungua kamba zake?
6 ni nyumba ya nani nimeifanya katika Araba, au nyumba yake katika nchi ya chumvi?
Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake, nchi ya chumvi kuwa makao yake.
7 Hucheka kwa dharau katika kelele katika mji; hasikilizi kelele za mwongozaji.
Huzicheka ghasia za mji, wala hasikii kelele za mwendesha gari.
8 Hutembeatembea juu ya milima kama malisho yake; huko hutafuta kila mmea ulio wa kijani kwa ajili ya kula.
Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho na kutafuta kila kitu kibichi.
9 Je nyati atakuwa na furaha kukutumikia? Je atakubali kukaa katika zizi lako?
“Je, nyati atakubali kukutumikia? Atakaa karibu na hori lako usiku?
10 Waweza kumwongoza nyati kulima mtaro kwa kamba? Je atachimba bonde kwa ajili yako?
Je, waweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba? Je, atalima mabonde nyuma yako?
11 Je waweza kumtumaini kwasababu ya nguvu zake nyingi? Je waweza kumwachia kazi yako ili aifanye?
Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi? Utamwachia yeye kazi zako nzito?
12 Je waweza kumtegemea akuletee nyumbani nafaka, au kukusanya nafaka katika uwanda wako wa kupuria?
Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?
13 Mabawa ya mbuni hupunga kwa majivuno, bali je mabawa na manyoya yana upendo?
“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha, lakini hayawezi kulinganishwa na mabawa na manyoya ya korongo.
14 Kwa maana huuacha mayai yake katika nchi, na huyaacha yapate joto katika mavumbi;
Huyataga mayai yake juu ya ardhi, na kuyaacha yapate joto mchangani,
15 husahau kuwa mguu waweza kuyaharibu au kwamba mnyama mwitu aweza kuyakanyaga.
bila kujali kuwa mguu waweza kuyaponda, kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.
16 Huyatendea vibaya makinda yake kana kwamba si yake; haogopi kwamba kazi yake yaweza kupotea bure,
Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake; hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,
17 kwasababu Mungu amemnyima hekima na hajampa ufahamu wowote.
kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima, wala hakumpa fungu la akili njema.
18 Na wakati anapokimbia kwa haraka, huwacheka kwa dharau farasi na mpanda farasi wake.
Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia, humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.
19 Je umempa farasi nguvu zake? Je umeivika shingo yake kwa manyoya?
“Je, wewe humpa farasi nguvu au kuivika shingo yake manyoya marefu?
20 Je umemfanya aruke kama panzi? Enzi ya mlio wake ni wa kutisha.
Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige, akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?
21 Hurarua kwa nguvu na kufurahia katika nguvu zake; hukimbia upesi kukutana na silaha.
Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake, husonga mbele kukabiliana na silaha.
22 Huidharau hofu na hashangazwi; huwa harudi nyuma kutoka katika upanga.
Huicheka hofu, haogopi chochote, wala haukimbii upanga.
23 Podo hugongagonga ubavuni mwake, pamoja na mkuki unaong'aa na fumo.
Podo hutoa sauti kando yake, pamoja na mkuki unaongʼaa na fumo.
24 Huimeza nchi kwa hasira na ghadhabu; katika sauti ya tarumbeta, hawezi kusimama sehemu moja.
Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi, wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.
25 Wakati wowote tarumbeta inapolia, husema, 'Ooh! Huisikia harufu ya vita kutoka mbali - vishindo vya radi za makamanda na makelele.
Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’ Hunusa harufu ya vita toka mbali, sauti ya mtoa amri na ukelele wa vita.
26 Je ni kwa hekima yako kwamba mwewe hupaa juu, na ya kuwa huyanyosha mabawa yake kwa upande wa kusini?
“Je, mwewe huruka kwa hekima yako na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?
27 Je ni kwa agizo lako kwamba tai huruka juu na kufanya kiota chake katika sehemu za juu?
Je, tai hupaa juu kwa amri yako na kujenga kiota chake mahali pa juu?
28 Huishi katika majabali na hufanya makao yake katika vilele vya majabali, na ngomeni.
Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku; majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.
29 Kutoka huko hutafuta mawindo; macho yake huyaona mawindo kutoka mbali.
Kutoka huko hutafuta chakula chake; macho yake hukiona kutoka mbali.
30 Makinda yake hunywa damu pia; na pale walipo watu wafu, ndipo na yeye alipo.
Makinda yake hujilisha damu, na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”