< Mwanzo 9 >
1 Kisha Mungu akambariki Nuhu na wanawe, na kuwaambia, “Zaeni, mkaongezeke, na muijaze nchi.
Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia.
2 Hofu na utisho wenu vitakuwa juu ya kila mnyama aliye hai juu ya nchi, juu ya kila ndege wa angani, juu ya kila kitu kiendacho chini juu ya ardhi, na juu ya samaki wote wa baharini. Vimetolewa katika mikono yenu.
Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu.
3 Kila kitu kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula kwa ajili yenu. Kama nilivyo wapa mimea, sasa nawapa kila kitu.
Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
4 Lakini msile nyama pamoja na uhai wake - yaani damu yake - ndani yake.
“Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai.
5 Lakini kwa ajili ya damu yenu, uhai uliomo katika damu yenu nitataka malipo. Kutoka katika mkono wa kila mnyama nitaitaka. Kutoka katika mkono wa kila mtu, yaani, kutoka katika mkono wa yule ambaye amemuua ndugu yake, nitataka fidia kwa ajili ya uhai wa mtu huyo.
Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.
6 Yeyote amwagaye damu ya mtu, kwa njia ya mtu damu yake itamwagwa, kwa sababu ilikuwa ni katika mfano wa Mungu kwamba Mungu alimuumba mtu.
“Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu.
7 Na hivyo nanyi zaeni na kuongezeka, sambaeni katika inchi yote na muongezeke juu yake.”
Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”
8 Kisha Mungu akazungumza na Nuhu na wanae pamoja naye, akisema,
Ndipo Mungu akamwambia Noa na wanawe pamoja naye:
9 “Kwa ajili yangu, sikiliza! Ninakwenda kulithibitisha agano langu pamoja nawe na uzao wenu baada yenu,
“Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu,
10 na kwa kila kiumbe hai kilicho pamoja nawe, pamoja na ndege, mnyama wa kufugwa, na kila kiumbe cha nchi pamoja nawe, kuanzia kwa wote waliotoka kwenye safina, mpaka kwa kila kiumbe hai juu ya nchi.
pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani.
11 Kwa sababu hii ninalithibitisha agano langu pamoja nanyi, kwamba hapatatokea kuangamizwa kwa mwenye mwili kwa njia ya maji ya gharika. Tena hapatatokea gharika ya kuangamiza nchi.”
Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”
12 Mungu akasema, “na hii ndiyo ishara ya agano ambalo ninafanya kati yangu na ninyi pamoja na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, kwa vizazi vyote vya baadaye:
Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo:
13 Nimeweka upinde wangu wa mvua katika wingu, na itakuwa ndiyo ishara ya agano kati yangu na nchi.
Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia.
14 Hata itakuwa nitakapoleta wingu juu ya nchi na upinde wa mvua ukaonekana katika wingu,
Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni,
15 ndipo nitakumbuka agano langu, ambalo ni kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai cha wote mwenye mwili. Maji hayatafanyika tena gharika kuharibu wote wenye mwili.
nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote.
16 Upinde wa mvua utakuwa katika mawingu na nitauona, ili kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na kila kiumbe hai cha wote wenye mwili ambacho kiko juu ya nchi.”
Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
17 Kisha Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ni ishara ya agano ambalo nimelithibitisha kati yangu na wenye mwili wote ambao wako juu ya nchi.”
Hivyo Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”
18 Wana wa Nuhu ambao walitoka katika safina walikuwa ni Shemu, Hamu, na Yafethi. Na Hamu akamzaa kanaani.
Wana wa Noa waliotoka ndani ya safina ni: Shemu, Hamu na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.)
19 Watatu hawa walikuwa ndio wana wa Nuhu, na kutokea kwa hawa nchi yote ikajaa watu.
Hawa ndio waliokuwa wana watatu wa Noa, kutokana nao watu walienea katika dunia.
20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, na akapanda mizabibu.
Noa akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu.
21 Akanywa sehemu ya divai na akalewa. Akawa amelala hemeani uchi.
Alipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake.
22 Kisha Hamu, baba yake na Kanaani, akaona uchi wa baba yake na akawaambia ndugu zake wawili waliokuwa nje.
Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.
23 Kwa hiyo Shemu na Yafethi wakachukua kanzu wakaitanda juu ya mabega yao, na wakatembea kinyumenyume na wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zikiwa zimegeuka nyuma upande mwingine, kwa hiyo hawakuona uchi wa baba yao.
Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.
24 Nuhu alipozinduka kutoka katika ulevi wake, alijua ni jambo gani mtoto wake mdogo amemfanyia.
Noa alipolevuka kutoka kwenye mvinyo wake na kujua lile ambalo mwanawe mdogo kuliko wote alilokuwa amemtendea,
25 Hivyo akasema, “Alaaniwe Kanaani. Na awe mtumishi kwa watumishi wa ndugu zake.”
akasema, “Alaaniwe Kanaani! Atakuwa mtumwa wa chini sana kuliko watumwa wote kwa ndugu zake.”
26 Akasema pia, Yahwe, Mungu wa Shemu, abarikiwe, Kanaani na awe mtumwa wake.
Pia akasema, “Abarikiwe Bwana, Mungu wa Shemu! Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
27 Mungu na apanuwe mipaka ya Yafethi, na afanye makazi yake katika hema za Shemu. Kanaani na awe mtumwa wake.”
Mungu na apanue mipaka ya Yafethi; Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu, na Kanaani na awe mtumwa wake.”
28 Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka miatatu na hamsini.
Baada ya gharika Noa aliishi miaka 350.
29 Siku zote za Nuhu zilikuwa ni miaka mia tisa na hamsini, na kisha alikufa.
Noa alikuwa na jumla ya miaka 950, ndipo akafa.