< 2 Wafalme 8 >

1 Basi, Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke ambaye alimfufulia mtoto wake. Akamwambia, “Inuka na uenede pamoja na nyumba yako, na uishi popote uwezapo katika nchi nyingine, kwa sababu Yahwe ameiita njaa ambayo itakuja katika hii nchi kwa miaka saba.”
Wakati huu, Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa, “Ondoka wewe na jamaa yako ukaishi mahali popote unapoweza kwa kitambo kidogo, kwa sababu Bwana ameamuru njaa katika nchi hii ambayo itadumu kwa miaka saba.”
2 Basi yule mwanamke akainuka na akatii lile neno la mtumishi wa Mungu. Akaenda na nyumba yake na kuishi kwenye nchi ya Wafilisti miaka saba.
Yule mwanamke akafanya kama vile yule mtu wa Mungu alivyosema. Yeye na jamaa yake wakaondoka na kwenda kuishi katika nchi ya Wafilisti kwa miaka saba.
3 Ikafika kama mwishoni mwa miaka saba yule mwanamke akarudi kutoka kwenye ile nchi ya Wafilisti, na kwenda kwa mfalme kumuomba nyumba yake na kwa ajili ya nchi yake.
Baada ya miaka saba, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti, akaenda kwa mfalme kumsihi kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.
4 Basi mfalme alikuwa anaongea na Gehazi yule mtumishi wa Mungu, akisema, “Tafadhali niambie yale mambo makubwa ambayo Elisha ameyafanya.”
Mfalme alikuwa anazungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, naye alikuwa amesema, “Hebu niambie mambo yote makuu yaliyofanywa na Elisha.”
5 Basi alipokuwa akimwambia yule mfalme jinsi gani Elisha alivyomfufua yule mtoto aliyekufa, huyo mwanamke ambaye mtoto wake aliyekuwa amefufuliwa akaja kumuomba yule mfalme kwa ajili ya nyumba yake na nchi yake. Gehazi akasema, “Bwana wangu, mfalme, huyu ndiye yule mwanamke, na huyu ndiye mtoto wake, ambaye Elisha amemfufua.”
Wakati Gehazi alipokuwa akimweleza mfalme jinsi Elisha alivyomfufua mtu, yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa na Elisha akaja ili amsihi mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, “Huyu ndiye huyo mwanamke, bwana wangu mfalme, na huyu ndiye mwanawe ambaye Elisha alimfufua.”
6 Wakati yule mfalme alipomuuliza yule mwanamke kuhusu mtoto wake, alimwelezea yule mfalme. Ndipo mfalme akamwagizia ofisa makini, akisema, “Mrudishie vyote vilivyokuwa vyake na mavuno yake yote ya kwenye mashamba tangu siku alipoondoka hadi sasa.”
Mfalme akamuuliza yule mwanamke kuhusu mambo hayo, naye akamweleza. Ndipo akaamuru afisa ashughulikie shauri lake na kumwambia, “Mrudishie huyu mwanamke kila kitu kilichokuwa mali yake, pamoja na mapato yote yaliyotokana na shamba lake tangu siku alipoondoka nchini hadi sasa.”
7 Elisha akaja Damaskasi ambako Ben Hadadi yule mfalme wa Shamu alikuwa anaumwa. Yule mfalme aliambiwa, “Yule mtu wa Mungu amekuja hapa.”
Elisha akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu ametoka mbali akapanda hadi hapa,”
8 Mfalme akamwambia Hazaeli, “Chukua zawadi kwenye mkono wako na uende ukakutane na mtu wa Mungu, na ukazungumze na Yahwe kupitia yeye, ukisema, “Je nitapona huu ugonjwa wangu?”
mfalme akamwambia Hazaeli. “Chukua zawadi na uende kumlaki huyo mtu wa Mungu. Muulize Bwana kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’”
9 Basi Hazaeli akaenda kuonana naye na kuchukua zawadi zake za kila kitu kizuri cha Damskasi, akabeba ngamia arobaini. Hivyo Hazaeli akaja na kusimama mbele ya Elisha na kusema, “Mtoto wako Ben Hadadi mfalme wa Shamu amenituma kwako, kusema, “Je nitapona huu ugonjwa?”
Hazaeli akaenda kumlaki Elisha, akiwa amechukua zawadi ya kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’”
10 Elisha akamwambia, “Nenda, kwa Ben Hadadi, 'Utapona hakika,' lakini Yahwe amenionyesha kwamba atakufa hahkika.”
Elisha akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini Bwana amenifunulia kwamba kweli atakufa.”
11 Basi Elisha akamtumbulia macho Hazaeli hadi alipojisikia aibu, na yule mtu wa Mungu akalia machozi.
Elisha akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu mpaka akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.
12 Hazaeli akauliza, kwa nini unalia, bwana wangu?” Akajibu, “Kwa sababu najua uovu ambao utakaoufanya kwa watu wa Israeli. Utazichoma moto ngome zao kwa moto, na utawaua vijana wao kwa upanga, kuwaseta vipande vipande watoto wao wachanga, na kuwapasua mimba zao wanawake wenye mimba.”
Hazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?” Elisha akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga, na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”
13 Hazaeli akajibu, Ni nani mtumwa wako, ambaye atafanya jambo hili kubwa? Yeye ni mbwa tu.” Elisha akajibu, “Yahwe amenionyesha kwamba utakuwa mfalme juu ya Shamu.”
Hazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu namna hiyo?” Elisha akamjibu, “Bwana amenionyesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”
14 Ndipo Hazaeli akamwacha Elisha na kuja kwa bwana wake, ambaye alimwambia, “Je Elisha alikwambiaje?” Akajibu, “Ameniambia kwamba utapona bila shaka.”
Kisha Hazaeli akamwacha Elisha na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamuuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.”
15 Basi siku ya pili yake Hazaeli akachukua blangeti na kulichovya kwenye maji, na kulitandaza kwenye uso wa Ben Hadadi hivyo akafa. Basi Hazaeli akawa mfalme katika sehemu sehemu yake.
Lakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akaingia mahali pake kuwa mfalme wa Aramu.
16 Katika mwaka wa kumi na tano wa Yoramu mwana wa Ahabu, mfalme wa Israeli, Yehoramu akaanza kutawala. Alikuwa mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. Alianza wakati Yehoshafati alikuwa mfalme wa Yuda.
Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda.
17 Yoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipoanza kutawala, na alitawala kwa mda wa miaka minane katika Yerusalemu.
Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka minane.
18 Yoramu akatembea kwenye njia ya huyo mfalme wa Israeli, kama walivyokuwa wakifanya kwenye nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa na binti wa Ahabu kama mke wake, na alifanya uovu usoni kwa Yahwe.
Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti wa Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Bwana.
19 Walakini, kwa sababu ya mtumishi wake Daudi, Yahwe hakutaka kuiharibu Yuda, tangu alipomwambia kwamba atampatia wazao.
Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, Bwana hakutaka kuiangamiza Yuda. Alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili ya Daudi na wazao wake milele.
20 Katika siku za Yoramu, Edomu akaasi kutoka chini ya mkono wa Yuda, na wakamfanya mfalme juu yao wenyewe.
Wakati wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe.
21 Basi Yehoramu akaenda na maamri jeshi na magari ya farasi yote. Ilitokea kwamba akaamka usiku na kushambulia na kuwazunguka Waedomu, waliokuwa wamemzunguka na wale maamri jeshi wa magari ya farasi. Ndipo wanajeshi wa Yehoramu wakakimbilia wajumbani kwao.
Basi Yehoramu akaenda Sairi pamoja na magari yake yote ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. Hata hivyo, jeshi lake likatorokea nyumbani mwao.
22 Hivyo Edomu aliasi dhidi ya utawala wa Yuda katika siku hizi. Libna pia aliasi katika kipindi hicho hicho.
Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo.
23 Kwa mambo mengine yamhusuyo Yehoramu, yote aliyoyafanya, je hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya mfalme wa Yuda?
Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehoramu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
24 Yehoramu akafa na kuzikwa pamoja na baba zake, na akalala pamoja na baba zake katika mji wa Daudi. Ndipo Ahazi mtoto wake akawa mfalme katika sehemu yake.
Yehoramu akalala pamoja na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa Yohoramu mwana wa Ahabu, mfalme wa Israeli, Ahazi mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.
Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
26 Ahazi alikuwa ana umri wa miaka ishirini na mbili wakati alipoanza kutawala; alitawala kwa mda wa mwaka mmoja katika Yerusalemu. Mama yake alikuwa anaitwa Athalia; alikuwa mtoto wa Omri, mfalme wa Israeli.
Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli.
27 Ahazia alitembelea katika nyumba ya Ahabu; alifanya yale yaliyo maovu katika uso wa Yahwe, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa ikifanya, kwa kuwa Ahazia alikuwa mkwe kwenye nyumba ya Aabu.
Akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, na kutenda maovu machoni pa Bwana, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.
28 Ahazia akaenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu, kupigana dhidi ya Hazaeli, mfalme wa Shamu, katika Ramath Geleadi. Washami wakamjeruhi Yoramu.
Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu.
29 Mfalme Yoramu akarudi ili auguzwe huko Yezreeli kwenye yale majeraha ambayo Washami walimpatia huko Rama. Wakati alipopigana dhidi ya Hazaeli mfalme wa Shamu. Hivyo Ahazi mwana wa Yehoramu, mfalme Yuda, akashuka kwa Yezreeli kumuona Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu Yoramu alikuwa amejeruhiwa.
Hivyo Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa na Waaramu huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

< 2 Wafalme 8 >