< 1 Timotheo 3 >

1 Usemi huu ni wakuaminika: Kama mtu anatamani kuwa Msimamizi, anatamani kazi njema. 2 Kwa hiyo msimamizi ni lazima asiwe na lawama. Ni lazima awe mume wa mke mmoja. Ni lazima awe na kiasi, busara, mwenye utaratibu, mkarimu. Ni lazima awe uwezo wa kufundisha. 3 Asiwe anatumia mvinyo, asiwe mgomvi, bali mpole, mwenye amani. Ni lazima asiwe mwenye kupenda fedha. 4 Inampasa kuwasimamia vema watu wa nyumbani mwake mwenyewe, na watoto wake imewapasa kumtii kwa heshima zote. 5 Maana ikiwa mtu hajui kuwasimamia watu wa nyumbani mwake mwenyewe, atalileaje kanisa la Mungu? 6 Asiwe mwamini mpya, ili kwamba asije akajivuna na kuanguka katika hukumu kama yule mwovu. 7 Lazima pia awe na sifa njema kwa wote walioko nje, ili asije akaanguka kwenye aibu na mtego wa mwovu. 8 Mashemasi, vilevile wanapaswa kuwa wenye kustahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili. Wasitumie mvinyo kupita kiasi au kuwa na tamaa. 9 Waweze kuitunza kwa dhamiri safi ile kweli ya imani iliyofunuliwa. 10 Wawe pia wamethibitishwa kwanza, halafu waweze kuhudumu kwa sababu hawana lawama. 11 Wanawake vivyo hivyo wawe wenye heshima. Wasiwe wasingiziaji. Wawe na kiasi na waaminifu kwa mambo yote. 12 Mashemasi ni lazima wawe waume wa mke mmoja mmoja. Lazima waweze kuwasimamia vema watoto wao na wa nyumbani mwao. 13 Kwa kuwa wale wanaotumika vizuri hupata msimamo mzuri na ujasiri mkubwa katika imani iliyo katika Kristo Yesu. 14 Ninaandika mambo haya kwako, na ninatumaini kuja kwako hivi karibuni. 15 Lakini ikiwa nitachelewa, ninaandika ili upate kujua namna ya kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambalo ni kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msaada wa kweli. 16 Na haipingiki kwamba kweli ya Uungu uliyofunuliwa ni mkuu: “Alionekana katika mwili, akathibitishwa na Roho, akaonekana na malaika, akatangazwa miongoni mwa mataifa, akaaminiwa na ulimwengu, na akachukuliwa juu katika utukufu.”

< 1 Timotheo 3 >