< Ufunuo 11 >
1 Ndipo nikapewa mwanzi uliokuwa kama ufito wa kupimia, nikaambiwa, “Nenda ukapime hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo.
2 Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu, uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu wa Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili.
3 Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku 1,260, wakiwa wamevaa nguo za gunia.”
4 Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Bwana Mungu wa dunia yote.
5 Kama mtu yeyote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu yeyote atakayetaka kuwadhuru.
6 Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo.
7 Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua. (Abyssos )
8 Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa, ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo pia Bwana wao alisulubiwa.
9 Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu wazikwe.
10 Watu waishio duniani watazitazama kwa furaha maiti za hao manabii wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu hao manabii waliwatesa watu waishio duniani.
11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.
12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama.
13 Saa iyo hiyo, kukatokea tetemeko kubwa la nchi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
14 Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.
15 Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema: “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” (aiōn )
16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,
17 wakisema: “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu na ukaanza kutawala.
18 Mataifa walikasirika nao wakati wa ghadhabu yako umewadia. Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa na kuwapa thawabu watumishi wako manabii na watakatifu wako pamoja na wale wote wanaoliheshimu Jina lako, wakubwa kwa wadogo: na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”
19 Ndipo hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.