< Zaburi 39 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi. Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”
2 Lakini niliponyamaza kimya na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka.
3 Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu:
4 “Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi.
5 Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi.
6 Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi.
7 “Lakini sasa Bwana, nitafute nini? Tumaini langu ni kwako.
8 Niokoe kutoka kwenye makosa yangu yote, usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.
9 Nilinyamaza kimya, sikufumbua kinywa changu, kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.
10 Niondolee mjeledi wako, nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.
11 Unakemea na kuadhibu wanadamu kwa ajili ya dhambi zao; unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo: kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
12 “Ee Bwana, usikie maombi yangu, usikie kilio changu unisaidie, usiwe kiziwi kwa kulia kwangu. Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni, kama walivyokuwa baba zangu wote,
13 Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”