< Zaburi 106 >

1 Msifuni Bwana. Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.
Msifuni Yahwe. Mshukuruni Yahwe, kwa kuwa ni mwema, kwa maana uaminifu wa agano lake wadumu milele.
2 Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Bwana au kutangaza kikamilifu sifa zake?
Ni nani awezaye kuyahesabu mataendo makuu ya yahwe au kutangaza katika ukamilifu sifa zote za matendo yake ya kuaminika.
3 Heri wale wanaodumisha haki, ambao daima wanafanya yaliyo mema.
Wamebarikiwa wale watendao yaliyo mema na matendo yao yaliyo haki siku zote.
4 Ee Bwana, unikumbuke unapowatendea mema watu wako, uwe msaada wangu unapowaokoa,
Ukumbuke, Ee Yahwe, unapowaonesha watu wako neema; unisaidie unapowaokoa.
5 ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako, niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako, na kuungana na urithi wako katika kukusifu.
Ndipo nitaona mafanikio ya wateule wako, wakifurahia katika furaha ya taifa lako, na utukufu pamoja na urithi wako.
6 Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda, tumekosa na tumetenda uovu.
Tumefanya dhambi kama babu zetu, tumekosea, na kufanya uovu.
7 Wakati baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, Bahari ya Shamu.
Baba zetu hawakuyatambua matendo yako ya ajabu katika Misri; walipuuzia matendo yako mengi ya uaminifu wa agano; waliasi penye bahari, bahari ya Shamu.
8 Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.
Hata hivyo, yeye aliwaokoa kwa ajili ya jina lake ili kwamba aweze kuzifunua nguvu zake.
9 Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.
Aliikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka. Kisha akawaongoza vilindini, kana kwamba ni jangwani.
10 Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.
Aliwaokoa kutoka mkononi mwa wale waliowachukia, na aliwaokoa kutoka mkononi mwa adui.
11 Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja.
Lakini maji yaliwafunika washindani wao; hakuna hata mmoja aliye okolewa.
12 Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake.
Ndipo waliyaamini maneno yake, nao waliimba sifa zake.
13 Lakini mara walisahau aliyowatendea, wala hawakungojea shauri lake.
Lakini walisahau haraka kile alichofanya; hawakuyasubiri maelekezo yake.
14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani.
Walikuwa na tamaa isiyotoshelezwa jangwani, wakamjaribu Mungu nyikani.
15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.
Aliwapa ombi lao, lakini alituma gonjwa ambalo lilishambulia miili yao.
16 Kambini walimwonea wivu Mose, na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Bwana.
Katika kambi wakawa na wivu juu Musa na Haruni, kuhani mtakatifu wa Yahwe.
17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake.
Nchi ilifunguka na ilimmeza Dathani na iliwafunika wafuasi wa Abiramu.
18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu.
Moto uliwaka kati yao; moto uliwaangamiza waovu.
19 Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma.
Walitengeneza ndama huko Horebu na kuabudu sanamu ya kuyeyuka.
20 Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani.
Wakaubadili utukufu wa Mungu kuwa mfano wa ng'ombe alaye majani.
21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyekuwa ametenda mambo makuu huko Misri,
Walimsahau Mungu wokozi wao, aliyefanya mambo makuu katika Misri.
22 miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu.
Alifanya matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu na matendo makuu penye Bahari ya Shamu.
23 Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Mose mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.
Mungu angetangaza uharibifu wao, kama sio Musa, mteule wake, aliingilia kati kugeuza hasira yake dhidi ya kuwaangamiza.
24 Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake.
Kisha waliidharau nchi yenye matunda; hawakuiamini ahadi yake,
25 Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii Bwana.
bali walilalamiaka katika mahema yao, na hawakumtii Yahwe.
26 Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani,
Kwa hiyo aliinua mkono wake na kuapa kwao kuwa atawaacha wafe jangwani,
27 kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote.
akitawanya uzao wao kati ya mataifa, na kuwatawanya katika nchi za kigeni.
28 Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.
Waliabudu Baal ya Poeri na walizila dhabihu zilizotolewa kwa wafu.
29 Waliichochea hasira ya Bwana, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao.
Walimkasirisha kwa matendo yao, na pigo la gonjwa baya liliwashambulia kati yao.
30 Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa.
Ndipo Finehasi aliinuka kuingilia kati, na pigo likakoma.
31 Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.
Ilihesabika kwake kama tendo la haki kwa vizazi vyote hata milele.
32 Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Bwana, janga likampata Mose kwa sababu yao;
Pia walimkasirisha Yahwe penye maji ya Meriba, na Musa aliteseka kwa ajili yao.
33 kwa maana walimwasi Roho wa Mungu, na maneno yasiyofaa yakatoka midomoni kwa Mose.
Walimghadhabisha Musa naye akaongea haraka.
34 Hawakuyaangamiza yale mataifa kama Bwana alivyowaagiza,
Hawakuyaharibu mataifa kama Yahwe alivyowaamuru,
35 bali walijichanganya na mataifa na wakazikubali desturi zao.
bali walichangamana na mataifa na walijifunza njia zao
36 Waliabudu sanamu zao, zikawa mtego kwao.
nao waliabudu sanamu, nazo zikawa mtego kwao.
37 Wakawatoa wana wao na binti zao dhabihu kwa mashetani.
Waliwatoa wana wao na binti zao kwa mapepo.
38 Walimwaga damu isiyo na hatia, damu za wana wao na binti zao, ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.
Walimwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana na binti zao, ambao waliwatoa kama dhabihu kwa sanamu za Kanaani, waliinajisi nchi kwa damu.
39 Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda; kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba.
Walinajisiwa kwa matendo yao; katika matendo yao walikuwa kama malaya.
40 Kwa hiyo Bwana akawakasirikia watu wake na akauchukia sana urithi wake.
Hivyo Yahwe aliwakasilikia watu wake, akawadharau watu wake mwenyewe.
41 Akawakabidhi kwa mataifa na adui zao wakawatawala.
Akawaruhusu mataifa, na wale walio wachukia wakawatawala.
42 Adui zao wakawaonea na kuwatia chini ya mamlaka yao.
Maadui zao wakawaonea, wakatiishwa chini ya mamlaka yao.
43 Mara nyingi aliwaokoa lakini walikuwa wamezama kwenye uasi, nao wakajiharibu katika dhambi zao.
Mara nyingi alienda kuwasaidia, lakini waliendelea kuasi nao walishushwa chini kwa dhambi zao wenyewe.
44 Lakini akaangalia mateso yao wakati aliposikia kilio chao;
Hata hivyo, aliiangalia dhiki yao aliposikia kilio chao kwa ajili ya msaada.
45 kwa ajili yao akakumbuka agano lake, na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake.
Alikumbuka agano lake pamoja nao na alijirudi kwa sababu ya upendo wake thabiti.
46 Akawafanya wahurumiwe na wote waliowashikilia mateka.
Aliwafanya wote waliowateka wawahurumie.
47 Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe. Tukusanye tena kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.
Utuokoe, Ee Yahwe, Mungu wetu. Utukusanye kutoka kati ya mataifa ili kwamba tuweze kulishukuru jina lako takatifu na utukufu katika sifa zako. Yahwe,
48 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Watu wote na waseme, “Amen!” Msifuni Bwana.
Mungu wa Israeli, na asifiwe toka milele na milele. watu wote walisema, “Amen.” Msifuni Yahwe. Kitabu cha tano.

< Zaburi 106 >