< Mambo ya Walawi 19 >

1 Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akazungumza na Musa, akisema.
2 “Sema na kusanyiko lote la Israeli na uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wenu, ni mtakatifu.
Zungumza na kusanyiko lote la watu wa Israeli na uwaambie, 'Ni lazima muwe watakatifu, kwa kuwa mimi Yahweh Mungu wenu ni mtakatifu.
3 “‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
Kila mtu amstahi mama yake na baba yake. Na ni lazima muzishike Sabato zangu. Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
4 “‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya shaba. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
Msizigeukie sanamu zisizo na thamani, wala kujitengenezea wenyewe miungu kutokana na chuma. Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
5 “‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa Bwana, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu.
Unapotoa dhabihu za sadaka ya ushirika kwa Yahweh, utatoa ili kupata kibali.
6 Sadaka hiyo italiwa siku iyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto.
Ni sharti iliwe siku hiyo hiyo uliyoitoa, au siku inayofuata.
7 Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa.
Kama kinabaki kitu cho chote hata siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto. Kama kitaliwa katika siku ya tatu kitakuwa najisi. Hakitakubalika,
8 Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa Bwana; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.
lakini kila akilaye ni lazima atachukua hatia yake kwa sababu amekivunjia heshima kilicho kitakatifu kwa Yahweh. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
9 “‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako.
Unapovuna mavuno ya ardhi yako, usivune hata pembezo mwa shamba lako kabisa, wala hutakusanya mabaki ya mavuno yako yote.
10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
Usikusanye kila zabibu kutoka katika mizabibu yako, wala usiziokote dhabibu zilizoanguka chini katika shamba la mizabibu. Ni lazima uziache kwa ajili ya masikini na kwa ajili ya wageni. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
11 “‘Usiibe. “‘Usiseme uongo. “‘Msidanganyane.
Usiibe. Usiseme uongo. Msidanganyane.
12 “‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
Usiape kwa jina langu kwa uongo na kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh
13 “‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako. “‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi.
Usimgandamize jirani yako wala kumwibia. Usishikilie malipo ya kibarua usiku kucha hata asubuhi.
14 “‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
Usimlaani kiziwi au kuweka kikwazo mbele ya kipofu. Badala yake, yakupasa umwogope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
15 “‘Usipotoshe haki; usionyeshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.
Usisababishe hukumu ikawa ya uongo. Usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni masikini na usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni mtu muhimu. Badala yake, amua juu ya jirani yako kwa haki.
16 “‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako. “‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Bwana.
Usiende huku na huko ukisema habari za uchochezi miongoni mwa watu wako, bali tafuta kuyalinda maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Yahweh.
17 “‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.
Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Mkemee jirani yako kwa heshima ili kwamba usishiriki katika dhambi kwa sababu yake.
18 “‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Bwana.
Usijilipize kisasi au kuwa na chuki yoyote dhidi ya mtu yeyote wa watu wako, lakini badala yake mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Yahweh.
19 “‘Mtazishika amri zangu. “‘Usiwaache wanyama wako wa kufugwa wakazaana na wengine wa aina tofauti. “‘Usipande mbegu za aina mbili katika shamba lako. “‘Usivae nguo iliyofumwa kwa nyuzi za aina mbili tofauti.
Shika amri zangu. Usiwazalishe wanyama wako kwa kutumia wanyama wa aina nyingine tofauti. Usichanganye aina mbili tofauti za mbegu unapopanda shamba lako. Usivae vazi lililofumwa kwa kutumia nyuzi za rangi mbili tofauti zilizochanganywa pamoja.
20 “‘Kama mwanaume anakutana kimwili na mwanamke ambaye ni msichana mtumwa aliyeposwa na mwanaume mwingine, lakini ambaye hajakombolewa wala hajapewa uhuru, lazima iwepo adhabu inayofaa. Hata hivyo hawatauawa, kwa sababu msichana alikuwa bado hajaachwa huru.
Yeyote anayelala na msichana mtumwa aliyeposwa na mume mwingine, lakini ambaye hajakombolewa au hajaachwa huru, lazima waadhibiwe. Hawatauawa kwa sababu yule msichana hakuwa huru.
21 Lakini huyo mtu lazima alete kondoo dume kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa ajili ya sadaka ya hatia kwa Bwana.
Ni lazima mtu huyo alete sadaka yake ya hatia kwenye ingilio la hema la kukutania—kondoo dume iwe sadaka ya hatia.
22 Kupitia kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana kwa ajili ya dhambi aliyotenda, naye atasamehewa dhambi yake.
Kisha kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kandoo dume mbele za Yahweh kutokana na dhambi aliyoitenda. Nayo dhambi iliyotendwa itasamehewa.
23 “‘Mtakapoingia katika hiyo nchi na kupanda aina yoyote ya mti wa matunda, hesabuni matunda yake kama yaliyokatazwa. Kwa miaka mitatu mtayahesabu kwamba yamekatazwa; hayaruhusiwi kuliwa.
Mtakapoingia katika nchi na kupanda aina zote za miti kwa chakula, kisha mtayahesabu matunda yatakayozaliwa kuwa yamekatazwa kuliwa. Tunda litakatazwa kwako kwa miaka mitatu. Halitaliwa.
24 Katika mwaka wa nne matunda yote ya mti huo yatakuwa matakatifu, sadaka ya sifa kwa Bwana.
Lakini katika mwaka wa nne matunda yote yatakuwa matakatiifu, matoleo ya sifa kwa Yahweh.
25 Bali katika mwaka wa tano mnaweza kula matunda ya mti huo. Kwa njia hii mavuno yenu yataongezewa. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
Katika mwaka wa tano unaweza kula tunda, ambalo umelisubiri ili kwamba mti uweze kuzaa zaidi. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
26 “‘Msile nyama yoyote yenye damu ndani yake. “‘Msifanye uaguzi wala uchawi.
Usile nyama yoyote amabayo damu ingalimo ndani yake. Usiulize kwa roho juu ya wakati ujao,
27 “‘Msikate nywele za kichwa denge, wala kunyoa pembe za ndevu zenu.
Usitafute kuwadhibiti wengine kwa njia ya nguvu za kichawi. Msifuate tabia za kipagani kama vile kunyoa denge au kunyoa pembe za ndevu zeu.
28 “‘Msichanje chale miili yenu kwa ajili ya mfu, wala msijichore alama juu ya miili yenu. Mimi ndimi Bwana.
Usiukate mwili wako kwa ajili ya wafu au kuchanja chale juu ya mwili wako. Mimi ndimi Yahweh.
29 “‘Usimdhalilishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo nchi itageukia ukahaba na kujaa uovu.
Usimwaibishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo taifa litaangukia kwenye ukahaba na nchi itajawa na uovu.
30 “‘Shika Sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Bwana.
Utazitunza Sabato zangu na kupaheshimu mahali patakatifu pa hema langu la kukutania. Mimi ndimi Yahweh.
31 “‘Msiende kwa waaguzi, wala msitafute wapunga pepo, kwa maana watawanajisi. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
Msiwageukie wale wanaoongea na wafu au roho wachafu. msiwatafute, la sivyo watawanajisi ninyi, Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
32 “‘Uwapo mbele ya mzee, simama ili kuonyesha heshima kwa wazee, nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
Ni lazima usimame mbele za mtu mwenye mvi na uheshimu uwepo wa mzee. Yakupasa umwegope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
33 “‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase.
Mgeni anapoishi miongoni mwenu katika nchi yanu, usimtendee lolote lililobaya.
34 Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
Mgeni anayeishi pamoja nanyi ni lazima awe kama mwenyeji Mwisraeli mzaliwa anayeishi kwenu, na sharti umpende kama unavyojipenda wewe mwenyewe, ni kwa sababu wewe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
35 “‘Usitumie vipimo vya udanganyifu unapopima urefu, kupima uzito, wala kupima wingi.
Unapopima urefu, uzito, au wingi usitumie vipimo vya udanganyifu.
36 Tumia mizani halali, mawe ya kupimia uzito halali, efa halali, na hini halali. Mimi ndimi Bwana Mungu wako, ambaye alikutoa katika nchi ya Misri.
Tumia mizani iliyo halali, mawe ya kupimia uzito yaliyo halali, efa halali, hini iliyo halali. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya utumwa ya Misri.
37 “‘Shika amri zangu zote na sheria zangu zote, nawe uzifuate. Mimi ndimi Bwana.’”
Utayatii maagizo yangu na sheria zangu zote na kuzitenda. Mimi ndimi Yahweh.

< Mambo ya Walawi 19 >