< 2 Samweli 16 >

1 Daudi alipokuwa amekwenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini na kiriba cha divai.
Daudi alipokuwa amekwenda kitambo juu ya kilele cha kilima, Siba mtumishi wa Mefiboshethi akaja kumlaki akiwa na punda wawili waliokuwa wamebeba vipande mia mbili vya mikate, vishada mia moja vya mizeituni, vishada mia moja vya tini na mfuko wa ngozi uliojaa mvinyo.
2 Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.”
Mfalme akamuliza Siba, “Kwa nini umeleta hivi vitu?” Siba akajibu, “punda ni kwa ajili ya familia yako kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya matumizi ya askari wako, na mvinyo ni kwa ajili kunywa watakaozimia nyikani.”
3 Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?” Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’”
Mfalme akauliza, “Na mjukuu wa bwana wako yuko wapi?” Siba akamjibu mfalme, “Tazama, yeye amesalia Yerusalemu kwa maana alisema, 'Leo nyumba ya Israeli itanirudishia ufalme wa baba yangu.”
4 Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.”
Kisha mfalme akamwambia Siba, “Tazama, yote yaliyomilikiwa na Mefiboshethi sasa yatakuwa yako.” Siba akajibu, “Nainama kwa unyenyekevu kwako bwana wangu mfalme. Na nipate kibari mbele zako.”
5 Mfalme Daudi alipokuwa anakaribia Bahurimu, mtu mmoja kutoka ukoo huo huo kama jamaa ya Sauli, akatoka humo, ambaye jina lake ni Shimei mwana wa Gera; akawa analaani alipokuwa akitoka.
Mfalme Daudi alipokaribia Bahurimu, akaja mtu kutoka katika ukoo wa Sauli, jina lake Shimei mwana wa Gera. Kadiri alivyokuwa akitembea alikuwa akilaani.
6 Akamtupia Daudi na maafisa wote wa mfalme mawe, ingawa vikosi vyote na walinzi maalum walikuwa kulia na kushoto mwa Daudi.
Akamrushia Daudi mawe na maofisa wa mfalme, bila kujali jeshi na walinzi wa mfalme waliokuwa kulia na kushoto mwa mfalme.
7 Shimei alivyokuwa akilaani, akasema, “Toka hapa, toka hapa, wewe mtu wa damu, wewe mtu mbaya kabisa!
Shimei akalaani, “Nenda zako, toka hapa, mwovu wewe, mtu wa damu!
8 Bwana amekulipiza kwa ajili ya damu yote uliyomwaga ya watu wa nyumba ya Sauli, ambaye nafasi yake umeimiliki wewe. Bwana amekabidhi ufalme mkononi mwa mwanao Absalomu. Maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mtu wa damu!”
Yahwe amelipa yote kwa ajili ya damu ya familia ya Sauli, ambaye unatawala badala yake. Yahwe ameweka ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao. Na sasa umeangamia kwa kuwa ni mtu wa damu.”
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.”
Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, “Kwa nini mbwa mfu anamlaani bwana wangu mfalme? Tafadhari niache niende nikamwondolee kichwa chake.”
10 Lakini mfalme akamwambia, “Mna nini nami, enyi wana wa Seruya? Ikiwa analaani kwa sababu Bwana amemwambia, ‘Mlaani Daudi,’ nani awezaye kuuliza, ‘Kwa nini unafanya hivi?’”
Lakini mfalme akasema, “Nifanye nini nanyi enyi wana wa Seruya? Pengine ananilaani kwa kuwa Yahwe amemwambia, 'Mlaani Daudi.' Nani sasa awezaye kumwambia, 'Kwa nini unamlaani mfalme.”
11 Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, yeye ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuuondoa uhai wangu. Je, si zaidi sana kwa huyu Mbenyamini! Mwacheni, acha alaani, kwa maana Bwana amemwambia afanye hivyo.
Hivyo Daudi akamwambia Abishai na watumishi wake wote, “Tazameni, mwanangu aliyezaliwa kutoka katika mwili wangu anatafuta uhai wangu. “Si zaidi sana mbenjamini huyu akatamani anguko langu? Mwacheni alaani, kwa maana Yahwe amemwamru kufanya hivyo.
12 Inawezekana kwamba Bwana ataona dhiki yangu na kunilipa mema kwa ajili ya laana ninayopokea leo.”
Huenda Yahwe akaangalia maangaiko niliyofungiwa, na kunirudishia mema kwa jinsi nilivyolaaniwa leo.”
13 Kwa hiyo Daudi na watu wake wakaendelea na safari yao barabarani, huku Shimei akiwa anatembea pembezoni mwa kilima sambamba na Daudi, huku akimlaani na kumtupia Daudi mawe na kumrushia mavumbi.
Hivyo Daudi na watu wake wakaendelea njiani wakati Shimei kando yake ubavuni mwa mlima, aliendelea kulaani na kumrushia mavumbi na mawe huku akienda.
14 Mfalme na watu wote aliokuwa pamoja nao wakafika kwenye kituo chao wakiwa wamechoka. Mfalme akajiburudisha hapo.
Kisha mfalme na watu wake wote wakachoka, na akapumzika wakati wa usiku walipopumzika wote.
15 Wakati huo, Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye.
Absalomu na watu wote wa Israeli waliokuwa pamoja naye wakaja Yerusalemu na Ahithofeli alikuwa pamoja naye.
16 Ndipo Hushai, Mwariki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!”
Ikawa Hushai Mwarki, rafiki yake Daudi, akaja kwa Absalomu, naye akamwambia Absalomu, “Mfalme aishi daima! mfalme aishi daima.
17 Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonyesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?”
Absalomu akamwambia Hushai, “Je huu ndiyo utiifu wako kwa rafiki yako? Kwa nini haukwenda pamoja naye?”
18 Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha, yeye aliyechaguliwa na Bwana, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na watu wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye.
Hushai akamwambia Absalomu, “Hapana! badala yake, yule ambaye Yahwe, watu hawa na watu wote wa Israeli wamemchagua huyo ndiye nitakaye kuwa upande wake na ndiye nitakaye kaa naye.
19 Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.”
Kwani ni nani ninayepaswa kumtumikia? Je sipaswi kutumika mbele za mwana? kama nilivyotumika mbele za baba yako ndivyo nitakavyofanya mbele zako”
20 Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe shauri lako. Tufanye nini?”
Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe shauri lako kuhusu tunachopaswa kufanya.”
21 Ahithofeli akamjibu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.”
Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nenda ulale na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza kasri, na waisraeli wote watasikia kwamba umekuwa kitu kinachonuka kwa baba yako. Kisha mikono ya wote walio pamoja nawe itatiwa nguvu.”
22 Kwa hiyo wakasimika hema kwa ajili ya Absalomu juu ya paa, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake mbele ya Israeli wote.
Hivyo wakatanda hema kwa ajili ya Absalomu juu ya kasri na Absalomu akalala na masuria wa baba yake mbele za Israeli wote.
23 Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.
Nyakati hizo ushauri aliokuwa akitoa Ahithofeli ulikuwa ni kama mtu anavyosikia kutoka katika kinywa cha Mungu mwenyewe. Hivyo ndivyo jinsi ushauri wa Ahithofeli ulivyoonekana kwa Daudi na Absalomu

< 2 Samweli 16 >