< 1 Samweli 13 >

1 Sauli alikuwa na miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na miwili.
Sauli alikwa na umri wa miaka [thelathini] alipoanza kutawala; alipokuwa ametawala Israeli kwa miaka [arobaini],
2 Sauli alichagua watu 3,000 kutoka Israeli; miongoni mwa hao watu 2,000 walikuwa pamoja naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli, nao watu 1,000 walikuwa pamoja na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao.
aliwachagua wanaume elfu tatu wa Israeli. Elfu mbili walikuwa pamoja naye huko Mikmashi na katika nchi ya milima ya Betheli, wakati huo wale elfu moja walikuwa pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini. Askari waliobaki aliwarudisha nyumbani, kila mtu hemani kwake.
3 Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!”
Yonathani akaishinda ngome ya jeshi la Wafilisti iliyokuwa Geba na Wafilisti wakasikia habari hiyo. Baadaye Sauli alipiga tarumbeta katika nchi yote, akisema, “Sikieni enyi Waebrania.”
4 Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, nao sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali.
Israeli yote imesikia kwamba Sauli ameipiga ngome ya Wafilisti, na pia kwamba Israeli imekuwa uvundo kwa Wafilisti. Ndipo askari wakaitwa kwa pamoja kuungana na Sauli huko Gilgali.
5 Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita 3,000, waendesha magari ya vita 6,000 na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki ya Beth-Aveni.
Wafilisti walijikusanya pamoja kupigana dhidi ya Waisraeli: magari elfu tatu, watu elfu sita wakuendesha magari, na majeshi mengi kama mchanga ufukoni mwa bahari. Wakapanda na kupiga kambi huko Mikimashi, mashariki mwa Beth aveni.
6 Watu wa Israeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katikati ya miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki.
Watu wa Israeli walipoona kuwa wapo katika matatizo -kwa maana watu walikata tamaa, wakajificha kwenye mapango, kwenye vichaka, kwenye miamba, kwenye visima na katika mashimo.
7 Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani mpaka nchi ya Gadi na Gileadi. Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu.
Baadhi ya Waebrania walipanda kwenda Yordani katika nchi ya Gadi na Gileadi. Lakini Sauli alibaki Gilgali, na watu waliomfuata wakitetemeka.
8 Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika.
Alisubiri kwa siku saba, muda uliopangwa na Samweli. Lakini Samweli hakufika huko Gilgali, na watu wakatawanyika mbali na Sauli.
9 Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa.
Sauli akasema, “Nileteeni sadaka ya kuteketezwa na sdaka ya amani.” Kisha akatoa sadaka ya kuteketezwa.
10 Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki.
Mara tu alipomaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa Samweli akawasili. Sauli akatoka nje wakutane na kumsalimia.
11 Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?” Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi,
Basi Samweli akasema, “Umefanya nini?” Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanaiacha, na kwamba umechelewa hukufika kwa muda uliopangwa, na kwamba Wafilisti wamekwisha jikusanya huko Mikmashi,
12 nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa Bwana.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.”
nikasema, 'Sasa Wafilisti watashuka dhidi yangu huko Gilgali, na sijaomba kibali cha BWANA.' Kwa hiyo nikajilazimisha mwenyewe kutoa sadaka ya kuteketezwa.”.
13 Samweli akasema, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya Bwana Mungu wako aliyokupa. Kama ungelitii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote.
Ndipo Samweli akamwambia Sauli, “Umetenda mambo ya kipumbavu. Hukuheshimu amri ya BWANA Mungu wako aliyokupatia. Kwa maana BWANA angeutengeneza utawala wako juu ya Israeli milele.
14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya Bwana.”
Lakini sasa utawala wako hautaendelea. BWANA ametafuta mtu anayekubaliwa na moyo wake, kwa sababu wewe hukutii alichokuamuru.”
15 Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu 600.
Ndipo Samweli akasimama akapanda kutoka Gilgali hadi Gibea ya Benyamini. Basi Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, idadi yao ilikuwa kama watu mia sita.
16 Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi.
Sauli, mtoto wake Yonathani, na watu waliokuwa pamoja nao, wakabaki Geba ya Benyamimni. Lakini Wafilisti wakapiga kambi huko Mikmashi.
17 Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali,
Wateka nyara makundi matatu wakaja kutoka kambi ya Wafilisti. Kundi moja likapinda kuelekea Ofra, hadi nchi ya Shuali.
18 kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa.
Kundi jingine likageuka kuelekea Bethholoni, na kundi jingine likaelekea katika mpaka kulikabili bonde la Seboimu kuelekea jangwani.
19 Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!”
Hakuna hata mhunzi aliyeonekana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walisema, “Waebrania wasije wakajitengenezea mapanga au mikuki.”
20 Hivyo Waisraeli wote huteremka kwa Wafilisti ili kunoa majembe ya plau, majembe ya mkono, mashoka na miundu.
Lakini Waisraeli wote huwa wakiteremka kwa Wafilisti, kila mtu kunoa jembe lake, sululu yake, shoka lake na mundu wake.
21 Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekeli kunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekeli kwa nyuma, mashoka na michokoo.
Gharama za kunoa ncha za majembe, sululu, mashoka na kunyoosha michokoo ilikuwa theluthi moja ya shekeli.
22 Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote aliyekuwa kambini na Sauli na Yonathani ambaye alikuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli tu na mwanawe Yonathani ndio waliokuwa navyo.
Hivyo siku ya vita, hakukuwa na mapanga au mikuki iliyoonekana katika mikono yoyote ya askali waliokuwa na Sauli na Yonathani; Ni Sauli na mtoto wake tu ndio walikuwa nazo.
23 Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi.
Vikosi vya Wafilisti wakatokeza katika nija ya Mikmashi.

< 1 Samweli 13 >