< 1 Nyakati 15 >
1 Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, kisha akasimamisha hema kwa ajili yake.
2 Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu Bwana aliwachagua kulibeba Sanduku la Bwana na kuhudumu mbele zake milele.”
3 Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la Bwana na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake.
4 Kisha Daudi akawakusanya pamoja wazao wa Aroni na Walawi:
5 Kutoka wazao wa Kohathi, Urieli kiongozi na ndugu zake 120,
6 Kutoka wazao wa Merari, Asaya kiongozi na ndugu zake 220.
7 Kutoka wazao wa Gershoni, Yoeli kiongozi na ndugu zake 130.
8 Kutoka wazao wa Elisafani, Shemaya kiongozi na ndugu zake 200.
9 Kutoka wazao wa Hebroni, Elieli kiongozi na ndugu zake 80.
10 Kutoka wazao wa Uzieli, Aminadabu kiongozi na ndugu zake 112.
11 Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu.
12 Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli hadi mahali ambapo nimetengeneza kwa ajili yake.
13 Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la Bwana mara ya kwanza, hata ikasababisha Bwana Mungu wetu kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.”
14 Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli.
15 Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Mose alivyoamuru sawasawa na neno la Bwana.
16 Daudi akawaambia viongozi wa Walawi kuwaweka ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi.
17 Basi Walawi wakawaweka Hemani mwana wa Yoeli; kutoka miongoni mwa ndugu zake, Asafu mwana wa Berekia; kutoka miongoni mwa ndugu zao Wamerari, Ethani mwana wa Kushaiya;
18 hawa ndio waliochaguliwa kuwa wasaidizi wao: Zekaria, Yaazieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu, Mikneya, pamoja na mabawabu Obed-Edomu na Yehieli.
19 Waimbaji Hemani, Asafu na Ethani walichaguliwa kupiga matoazi ya shaba;
20 Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya walikuwa wapiga zeze kufuatana na sauti ya alamothi,
21 na Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-Edomu, Yehieli na Azazia walikuwa wapiga vinubi, wakiongozwa kwa kufuata sauti ya sheminithi.
22 Kenania kiongozi wa Walawi alikuwa msimamizi wa uimbaji; huu ndio uliokuwa wajibu wake kwa sababu alikuwa stadi katika hilo.
23 Berekia na Elikana walikuwa mabawabu kwa ajili ya Sanduku.
24 Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, makuhani, walikuwa wapiga tarumbeta mbele ya Sanduku la Mungu. Obed-Edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa mabawabu wa Sanduku.
25 Basi Daudi pamoja na wazee wa Israeli na majemadari wa vikosi vya elfu wakaenda ili kulipandisha Sanduku la Agano la Bwana kutoka nyumba ya Obed-Edomu kwa shangwe.
26 Kwa sababu Mungu alikuwa amewasaidia Walawi waliokuwa wanalichukua Sanduku la Agano la Bwana, mafahali saba na kondoo dume saba walitolewa dhabihu.
27 Basi Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, kama walivyokuwa wamevaa Walawi wote waliokuwa wanalichukua lile Sanduku, waimbaji nao walivaa vivyo hivyo, pamoja na Kenania aliyekuwa anaongoza nyimbo za waimbaji. Daudi alivaa pia kisibau cha kitani safi.
28 Hivyo Israeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Bwana kwa shangwe, wakipiga pembe za kondoo dume, tarumbeta, matoazi, wakipiga zeze na vinubi.
29 Sanduku la Agano la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akicheza na kusherehekea, akamdharau moyoni mwake.